Ruzuku ya Mbolea yazidi kupaisha kilimo Mbeya

Mwandishi Wetu,

Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Gidion Gilberty Mapunda, amesema zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wa halmashauri hiyo wanajihusisha na kilimo, huku asilimia 75 ya uchumi wa halmashauri ukitegemea kilimo, ufugaji na uvuvi.

Amesema maboresho ya utekelezaji wa mpango wa ruzuku nchini umerahisishia wakulima upatikanaji wa pembejeo kutokana na kuongezeka kwa mawakala katika kata 28 za wilaya hiyo. 

Ameishukuru serikali kwa kutoa ruzuku za pembejeo ambazo zimeongeza tija kwa wakulima huku akibainisha kuwa, msimu wa kilimo 2024/2025 Halmashauri iliweka malengo ya kuzalisha tani 230,000 za mahindi ambapo lengo limevukwa kwa kuzalisha tani 268,574 ikiwa ni sawa na asilimia 116 za lengo.

Akizungumzia upande wa zao la ngano Bw. Mapunda amesema uzalishaji umezidi matarajio kwa asilimia 139 ambapo halmashauri ilijiweea malengo ya kuzalisha tani 11,232 na ikavuka lengo kwa kuzalisha tani 15,692. 

Aidha, uzalishaji wa viazi mviringo ulivuka lengo kwa kuzalisha tani 325,381 dhidi ya lengo la tani 312,726 lililowekwa na halmashauri hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 104 ya uzalishaji.

Mapunda amesema mafanikio hayo yanatokana na utekelezaji wa mpango wa mbolea za ruzuku unaokwenda sambamba na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na mbegu bora inayotolewa na serikali kupitia TFRA.

Ameeleza kuwa, kutokana nahistoria ya matumizi ya mbolea katika halmashauri na mkoa huo, hakuna changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwani wakulima wamehamasika kutumia mbolea na mbolea zinapatikana katika kata zote za wilaya hiyo.

Katika kuboresha huduma kwa wakulima, Wizara ya Kilimo imewawezesha mabwana shamba kwa kuwapatia vitendea kazi ikiwa ni vishikwambi 83, vipima udongo na vingine vingi vinavyowasaidia kutoa ushauri wa kitaalam na kusajili wakulima kwa haraka.

Kwa upande wake, Mkulima Musa Robert Syunje kutoka kijiji cha Mwashiwawala, kata ya Iwindi, amesema amenufaika kwa asilimia 100 na mbolea za ruzuku na kuona mavuno yakiongezeka.

Ameeleza kuwa, kabla ya kuwepo ruzuku ya mbolea mfuko wa mbolea wa kilo 50 uliuzwa kwa Shilingi 120,000 hadi 130,000, lakini sasa wanapata kwa Shilingi 75,000.




Post a Comment

Previous Post Next Post