RUZUKU YA MBOLEA YAPAISHA UZALISHAJI, BEI YA KAHAWA RUVUMA

 Mwandishi Wetu,

Imeelezwa kuwa uzalishaji wa kahawa umeongezeka kutoka tani 25,000 msimu wa mwaka 2023/24 hadi tani 27,000 msimu wa mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la tani 2500 za kahawa kwa msimu katika Wilaya ya Mbinga.   

Ongezeko la uzalishaji huo limechochewa na matumizi sahihi ya mbolea za ruzuku zilizowapunguzia wakulima gharama za uzalishaji wa kahawa, kuongeza mavuno yenye ubora na kuleta ushindani sokoni.

Akizungumza ofisini kwake meneja wa Bodi ya Kahawa Kanda ya Ruvuma Rashidi Abilahi, amesema kuongezeka kwa uzalishaji wa Kahawa kunakwenda sambamba na ongezeko la bei ya Kahawa ghafi kutoka shilingi elfu tano kwa kilo mwaka 2022/23 hadi shilingi elfu tisa msimu wa mwaka 2024/2025

Ameongeza kuwa kwasasa wakulima wa kahawa wanaendelea kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali ikiwemo upatikanaji wa pembejeo za ruzuku, miche ya kahawa, bei ya kuridhisha kwa wakulima wanaouza kahawa ghafi pamoja na kadi janja ya mkulima.

Abilahi amefafanua kuwa tija  ya kahawa na ongezeko la bei vimechangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea ya ruzuku, ambapo mkulima aliyetumia mbolea kwa usahihi aliweza kuzalisha kahawa nyingi yenye ubora, na kuleta ushindani wa bei sokoni.

Akizungumzia bei ya kahawa ghafi msimu ujao unaotarajiwa kufunguliwa Julai mosi, Abilahi amesema kuwa Bodi ya Kahawa imeshatoa bei elekezi ambapo kilo moja ya kawaha ghafi ya majumbani itauzwa shilingi elfu tisa na kahawa ya mtamboni itauzwa kwa shilingi elfu 11500 kwa kilo.

Bodi ya Kahawa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wanashirikiana kutekeleza zoezi la usajili wa wakulima wa kahawa kunufaika na kadi janja ya mkulima na uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwenye zao hilo ili kuongeza tija, ambapo takribani wakulima wa kahawa 45,000 wanatarajiwa kuhakikiwa kwa kuhuisha taarifa zao kwenye mfumo wa pembejeo za ruzuku



Post a Comment

Previous Post Next Post