Rais Samia aridhishwa na kasi ya Aweso. Asema hana shaka na kufikiwa kwa lengo la CCM

Na Mwandishi Wetu,

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Wizara ya Maji kwa kusimamia na kuhakikisha lengo lililoainishwa  katika ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuwafikishia huduma ya maji Watanzania inafikiwa.

Pongezi hizo amezitoa wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Mtyangimbole wilayani Madaba kwa niaba ya miradi mingine 30 inayoendelea mkoani Ruvuma zoezi ambalo lilienda sambamba na kupokea taarifa ya uchimbaji wa visima 900 vya maji nchini.

Amesema anaridhishwa na utendaji wa Wizara ya Maji inayosimamiwa na Waziri Jumaa Aweso (Mb) pamoja na Katibu Mkuu Mhandisi Mwajuma Waziri kutokana na maendeleo ya sekta ya maji ambayo sasa yanaonekana sehemu mbalimbali nchini. 

Amesema ilani ya Chama cha Mapinduzi inaitaka wizara hiyo kuhakikisha inafikisha huduma ya maji kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini lakini mwenendo wa wizara unaonesha kuwa hadi kufikia mwaka 2025 huduma hiyo itakuwa imevuka malengo.

Aidha, Dkt. Samia amemuagiza Waziri Aweso kuhakikisha mradi huo wa Mtyangimbole unakamilika ndani ya miezi mitatu ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi wa maji wa Mtyangimbole pamoja na program ya uchimbaji wa visima 900, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema hadi sasa utekelezaji wa programu hiyo inayokusudia kuchimba visima  vitano kwa kila jimbo la uchaguzi nchini umefanikiwa kukamilisha visima 254 huku visima vingine vikiendelea kuchimbwa sehemu mbalimbali nchini,

Naye Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema utekelezaji wa miradi ya maji nchini unakwenda vizuri na kwamba wizara haitakuwa kikwazo katika kuhakikisha lengo la serikali linafikiwa kwa wakati.’



Post a Comment

Previous Post Next Post