Ameyasema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Magharibi, Mhe. Omary Massare aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupanda mazao yanayopendwa na wanyama waharibifu hifadhini kwa lengo la kuzuia wanyamapori hao kuingia kwenye makazi ya watu.
Mhe. Masanja amefafanua kuwa kumekuwa na changamoto ya ongezeko la matukio ya wanyamapori kuingia kwenye makazi ya watu na kusababisha madhara kwa wananchi na mali zao kutokana na wananchi kuingilia maeneo ya hifadhi.
“Changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kuingia kwenye makazi ya watu imesababishwa na uanzishwaji wa shughuli za kibinadamu kwenye shoroba, maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori na maeneo ya pembezoni mwa hifadhi” Mhe. Masanja amesisitiza.
Ameweka bayana kuwa kupanda mazao katika hifadhi za wanyamapori hakuwezi kuzuia wanyamapori kuhama kutoka mfumo mmoja wa ikolojia kwenda mfumo mwingine kwa sababu ya kiikolojia.
Aidha, kuhusu kifuta jasho/machozi kwa wananchi walioharibiwa mazao Wilayani Manyoni, Mhe. Masanja amesema tathmini itafanyika kwa wananchi ambao bado hawajalipwa kifuta jasho/machozi walipwe.
Mhe. Masanja amesema ili kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, Serikali inaendelea kuongeza nguvu kazi kwa kuajiri askari wa uhifadhi na pia kujenga vituo vya askari kwenye maeneo yenye changamoto.