JKCI Yaja Na Kampeni Ya Kuhamasisha Jamii Kufanya Mazoezi Kujikinga Na Magonjwa Ya Moyo

 

Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inatarajia kuanzisha matembezi ya kilomita tano kwa ajili ya kuhamasisha jamii kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi duniani.

Akizungumza wakati wa kupokea Tshirt 100 zilizotolewa na Kampuni ya Ulinzi ya K4S Security leo jijini Dar ers Salaam ambazo zitavaliwa katika matembezi hayo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema wameamua kuanzisha matembezi hayo ili kuihamasisha jamii kuona umuhimu wa kufanya mazoezi na kijikinga na magonjwa hayo.

Dkt. Kisenge aliishukuru kampuni hiyo kwa kuwa sehemu ya kuhamashisha jamii kujikinga na magonjwa ya moyo na kusema kuwa JKCI ina wajibu wa kuhakikisha jamii inajikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo ambayo yamekuwa yakisababisha vifo vya watu wengi duniani.

“Katika kuhakikisha jamii inakuwa salama Taasisi yetu hivi karibuni inatarajia kuanzisha matembezi ambayo yatatoa motisha kwa jamii kufanya mazoezi kama njia mojawapo ya kujikinga na magonjwa hayo,”.

“Tunatarajia kufanya matembezi ya kilomita tano angalau mara moja kwa mwezi, matembezi ambayo yatahamasisha wananchi wakiwemo wafanyakazi wetu kufanya mazoezi kwani moja ya kinga ya magonjwa ya moyo ni pamoja na kufanya mazoezi,”alisema Dkt.Kisenge.

Dkt. Kisenge aliongeza kuwa magonjwa ya moyo yanaweza kuzuilika kama jamii itafuata mtindo bora wa maisha ikiwemo kufanya mazoezi, kutokutumia bidhaa za tumbaku, kula mlo bora pamoja na kuacha kutumia vilevi ambavyo ni hatari kwa afya ya moyo.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ulinzi ya K4S Security Kemmy David alisema kampuni hiyo imeona ni vizuri kurudisha kwa jamii mafanikio wanayoyapata wakiwa na lengo la kusaidia jamii ili iweze kujikinga na magonjwa ya moyo.

“Hii ni mara yetu ya pili kama kampuni ya K4S Security kushirikiana na JKCI kuhakikisha jamii inayotuzunguka inafaidika na uwepo wetu kwani bila wao sisi tusingeweza kupata mafanikio tuliyonayo,”alisema David.

Meneja huyo alisema siku ya uzinduzi wa matembezi hayo wafanyakazi wa K4S Security watakuwa sehemu ya matembezi ili nao wajijengee tabia ya kufanya mazoezi kujilinda na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.

Matembezi hayo ambayo yana kauli mbiu ya “Fanya Mazoezi na JKCI, Linda Moyo Wako” yanayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni yatahusisha wafanyakazi wa Taasisi hiyo pamoja na wadau wengine wa afya.

Post a Comment

Previous Post Next Post