Na John Mapepele.
Naibu Katibu Mkuu wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu amesema Serikali imefanya mapinduzi na maboresho kwenye eneo la Hakimiliki miliki kwa wasanii ili waweze kunufaika na kazi zao.
Yakubu ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akihutubia kwenye kongamano la wadau wa muziki barani Afrika la ACCES katika tamasha lililoanza jana linalojumuisha wanamuziki kutoka nchi mbalimbali kwenye Bara la Afrika.
Amesema kutokana na mabadiliko ya kisheria yaliyofanyika hivi karibuni wanamuziki wa kitanzania watakwenda kufaidika na matumizi ya kazi zao.
Amesema tayari Serikali imeanza kutoa mirahaba kwa kazi zote za wasanii zinazotumika ambapo ameahidi kuwa serikali itaendelea kuwasaidia wasanii ili waweze kunufaika na kuchangia katika uchumi wa nchi.
Aidha, amefafanua kuwa dhamira ya Serikali ni kuendelea kushirikiana na wadau wote wa Sanaa ikiwa ni pamoja na ACCES ili kuendeleza na kuwasaidia wanamuziki na wasanii kwa ujumla.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha takribani juma moja sasa Tanzania na Afrika Kusini zinashirikiana kufanya Tamasha maalum la msimu wa utamaduni wa Afrika Kusini kwa lengo hilo hilo la kubadilishana uzoefu na kuinua vipaji.
Amewakaribisha wadau wote waliofika kwenye Kongamano hili kuhudhuria maonesho ya Sanaa yanayoendelea kufanyika makumbusho ya Taifa usiku wa leo.