Mhe.Mchengerwa afanya ziara BASATA, ampa maelekezo mahususi, Dkt. Mapana

Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amemtaka Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa *(BASATA)* nchini  Dkt. Mapana kurudisha hadhi ya sekta ya Sanaa nchini kwa kuweka mikakati itakayosaidia kukuza sekta na kuchangia mapato ya wasanii na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Julai 12, 2022 alipotembelea Ofisi ya BASATA  na kutoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu huyo wa BASATA aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan.

Baadhi ya maelekezo ambayo ametaka yafanyiwe kazi mara moja ni pamoja na kuziba mianya yote ya rushwa na upotevu wa mapato ambapo amesisitiza kuwa endapo utadhitiwa utasaidia kuongeza fedha nyingi Serikalini.

Pia amemtaka kuwa mbunifu wa mambo katika kuongoza taasisi hiyo ili kuja na mapinduzi chanya katika sekta hiyo.

"Katika wakati wa sasa ni muhimu kuipanga taasisi yako na kuwa na wataalam bobezi kwenye kila eneo kama wachumi, wataalam wa masoko, sheria na kadhalika ili kupiga hatua za kimataifa" amefafanua, Mhe. Mchengerwa


 Ameelekeza kuwaunganisha wasanii ili waweze kufanya kazi kwa kushirikiana  ili kupata wasanii wengi watakaokwenda katika ngazi za kimataifa kuliko hali ilivyo sasa ya kuwepo kwa wasanii wachache wanaitamba kimataifa.

Kuhusu kusimamia haki na maudhui pamoja na maadili, Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa BASATA ni chombo chenye mamlaka kisheria ya kusimamia hili hivyo kuwataka kusimamia kikamilifu.

Pia amesema Serikali inakwenda kuratibu tamasha la muziki Agosti mwaka huu.

Kwa upande wake  Dkt. Kedmon Mapana amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kuongoza BASATA na kuahidi kufanya kazi kwa weledi.

Aidha, amesema amepokea  maelekezo yote ya Waziri Mchengerwa na atayatekeleza mara moja ili kupiga hatua.

Post a Comment

Previous Post Next Post