MCHENGERWA:SERIKALI KUBORESHA SEKTA YA FILAMU NCHINI





  

***************

Na Thomas Nyindo, Bagamoyo

Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo imekuja na nguvu kubwa ili kuleta maboresho na mabadiliko ya kisasa katika ukuaji wa Sekta ya Filamu nchini.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Mohammedi Mchengerwa alipotembelea Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).

Mhe. Waziri ambaye aliongozana na viongozi kutoka Kampuni ya Nichani ya India ikiongozwa na Bw. Manu Nichani na Trans Innova ya Marekani ikiongozwa na Dkt. David Faria, amesema lengo la kuja kwa viongozi hao ni kuona namna gani wanaweza kutusaidia kufanya mabadiliko ya pamoja na kupata uzoefu katika sekta ya filamu.

“Dhamira ya Serikali ni kuleta mapinduzi ya dhati katika Sekta ya Filamu na tumedhamiria kweli kweli kuitoa hapa ilipo na kuipeleka mbele zaidi,” alisema Mhe. Mchengerwa.

Mhe. Waziri amesema Wizara kupitia mashirikiano baina ya Kampuni hizo mbili itafanya mambo makubwa ambayo watanzania watayafurahia na yatadumu kwa kizazi cha leo na cha baadae.

Mhe. Waziri amesema, wataalam hao wanampango wa kukutana wa waigizaji wa filamu nchini ili nao wapate uzoefu wa namna ya kuzalisha filamu au tamthilia.

“Wenzetu hawa wametupa uhakika wa kutusaidia katika kupata masoko, kutangaza kazi zetu na kuzifanya ziwe za kimataifa zaidi, amesema Mhe. Mchengerwa.

Mhe. Mchengerwa amesema ziara hio ilikua muhimu kwasababu itakua na manufaa kwetu ili wenzetu hao waweze kutusaidia kutuvusha hapa tulipo na kwenda mbele zaidi.
Mhe. Waziri amesema kama nchi tunataka tuwe miongoni mwa mataifa ambayo yako mbele zaidi katika kuandaa filamu.

“Tutaendelea kuwatia moyo waandaaji wa filamu, tutawatia moyo waigizaji wa filamu na wazalishaji wa filamu, lakini pia wanunuzi wa filamu ili kwa pamoja tuweze kufanikisha wazo na maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria Kuhakikisha Wizara hii inaleta furaha na faraja kwa Watanzania,” amesema Mhe. Waziri.

Naye Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye amesema TaSUBa inapata nguvu kubwa ya kusonga mbele kutokana na ushirikiano na uwezeshwaji mkubwa ambao Chuo kinapata kutoka kwa Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo.

Post a Comment

Previous Post Next Post