TFRA yapongezwa usimamizi ujenzi maabara ya mbolea

 Na Mwandishi Wetu,

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde ameipongeza Mamlaka Ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania kwa kuendelea kutekeleza jukumu lake la udhibiti wa mbolea huku ikitekeleza jukumu la ujenzi wa maabara ya mbolea ya kimataifa.

Mavunde ametoa pongezi hizo leo alipotembelea Ofisi za mamlaka hiyo ili kukagua maendeleo ya ujenzi wa maabara hiyo inayotarajia kukamilika mwezi Mei, 2022 mradi uliopo katika eneo la kilimo C wilayani Temeke Jijini Dar es Salaam.

Mavunde amesema pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Mamlaka ni vema mamlaka hiyo ikafanya manunuzi ya vifaa vyote vya ujenzi mapema ili mkandarasi asikwame katika ujenzi kutokana na kukosa vifaa hivo.

"Zipo njia za kurahisisha masuala ya manunuzi  bila kuathiri matakwa ya kisheria wasilisha mahutaji na ratiba yako kwa ajili ya ujenzi ili mamlaka iandae mahitaji hayo mapema" Mavunde alikazia.

Amesema, ujenzi wa maabara hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika kuboresha mazingira ya  kusimamia na kudhibiti ubora wa mbolea nchini.

Akizungumzia manufaa ya maabara hiyo, Mavunde amesema maabara inayojengwa itawasaidia wadau wa mbolea katika kupata majibu ya uchambuzi kwa wakati aidha itapunguza gharama ya mbolea kutokana na bei ya bidhaa hiyo kuongezeka kutokana na kucheleweshwa kwa majibu ya uchambuzi yaliyokuwa yakifanywa na vyombo binafsi na hivyo kuongeza gharama ya kutunza mzigo huo bandarini.

Akizungumza kuhusu bei ya mbolea Mhe. Mavunde  ameishukuru mamlaka kwa miongozo na ushauri  inayotoa kwa serikali  ikiwa ni pamoja na kushauri na kusimamia ujenzi wa  kiwanda cha mbolea  intracom Jijini Dodoma.

Amesema ujenzi wa kiwanda umefikia asilimia 65 huku kikitarajiwa  kuanza uzalishaji wa tani 6000 za mbolea  kwa mwaka ifikapo mwezi wa Julai na hivyo kupunguza mzigo wa gharama ya mbolea kwa wakulima.

Akizungumzia kuhusu maabara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Dkt. Stephan Ngailo amesema maabara hiyo  itakuwa na viwango vya kimataifa na ni maabara pekee Afrika Mashariki na Kati katika upimaji wa sampuli za mbolea.

Amesema mara ujenzi wake utakapokamilika mamlaka itahakikisha maabara hiyo  imepata ithibati ya kimataifa ili uchambuzi wake ukubalike duniani kote na mbolea inayopimwa katika maabara hiyo itambulike kwa ubora wake.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi,  Bi. Mwahija Irika alisema ujenzi huo umefikia asilimia 51 ambapo ujenzi wa kuta na umwagaji zege la juu katika floor ya kwanza umekamilika.

Amesema, nguzo katika ghorofa ya pili zimekamilika na kwamba kazi inayoendelea kwa sasa ni ufungaji wa marine board na mbao kwa ajili ya kumwaga zege katika ghorofa ya kwanza.

Akihitimisha taarifa yake Bi. Mwahija aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa juhudi kubwa za kuisaidia mamlaka kupata eneo la ujenzi pamoja na ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.

    Naibu Waziri wa Kilimo,Antony Mavunde  akizungumza na Waandishi wa     habari,baada ya kukagua Ujenzi wa Mahabara ya Mbolea.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania(TFRA),Dk Stephan Ngailo, akizungumza na waandishi wa habari Mara baada ya kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Mahabara ya Mbolea.

Post a Comment

Previous Post Next Post