WACHEZAJI 30 WA NGORONGORO HEROES U20 WAFANYIWA UCHUNGUZI WA MOYO

 

Mtaalam wa maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jesca Mlay akimtoa damu kapteni wa timu ya taifa chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes  Kelvin John kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya ya mwili wakati wachezaji 30 wa timu hiyo walivyofika katika taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya ya moyo kabla ya kushiriki mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchini Mauritania mwezi Februari mwaka huu.

Fundi sanifu wa moyo (Cardiovascular technologist) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Paschal Kondi akimpima mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography – ECG) mchezaji wa timu ya taifa chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes Kimwe Kisare wakati timu hiyo ilivyofika JKCI kwa ajili ya kuwafanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo kabla ya kushiriki mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchini Mauritania mwezi Februari mwaka huu.

Daktari binga wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aika Nkya akimpima jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph) mchezaji wa timu ya taifa chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes Nassor Saadun Hamoud  wakati timu hiyo ilivyofika JKCI kwa ajili ya kuwafanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo kabla ya kushiriki mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchini Mauritania mwezi Februari mwaka huu.

Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes wakiwa katika foleni ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Wachezaji 30 wa timu hiyo walifanyiwa vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, umeme wa moyo unavyofanya kazi na damu ikiwa ni mojawapo ya kutekeleza sheria ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kila mchezaji anayeshiriki mashindano hayo kupima.

Picha na: JKCI

……………………………………………………………………..

Wachezaji 30 wa timu ya Taifa chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes wamefanyiwa uchuguzi wa kina wa magonjwa ya moyo kama Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) linavyoelekeza kabla ya kuanza kwa mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ni lazima wachezaji wanaoshiriki mashindano hayo wapimwe afya zao.

Vipimo walivyofanyiwa wachezaji hao ni vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph), mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography –ECG), na vipimo mbalimbali vya damu kuangalia afya ya mwili kwa ujumla. Upimaji huu umefanywa na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Vipimo vya damu vilivyofanywa kwa wachezaji hao ni pamoja na kuangalia kama kuna maambukizi yoyote kwenye damu, kipimo cha kuangalia viwango vya mafuta katika mwili, kuchunguza madini ya chumvi mwilini na kipimo cha kuangalia kiwango cha sukari mwilini.

Matokeo ya vipimo hivyo yatasaidia kufahamu afya za wachezaji na utimamu wao wa kimwili kabla ya kwenda kushiriki katika mashindano ya AFCON yanayotarajia kuanza tarehe 14/02/2021 huko nchini Mauritania.

Tunatoa wito kwa vilabu vya mpira hapa nchini kuwaleta wachezaji wao kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo hii itawasaidia wachezaji hao kufahamu kama wanamatatizo au la na kuepukana na vifo vya ghafla vinavyoweza kuwapata wakiwa uwanjani. Kwa upande wa wananchi kabla ya kujiunga na vilabu vya mazoezi ni muhimu wakapima afya zao yakiwemo magonjwa ya moyo

Post a Comment

Previous Post Next Post