Watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA) wametakiwa kusimamia Sheria za Uhifadhi ili kunusuru maisha ya Wanyamapori ambao wamekuwa wakidhuriwa na Wananchi wanaovamia Mapori ya Akiba na Hifadhi kwa kufanya ujangili.
Agizo hilo limekuja kufuatia kuwepo kwa wimbi la Wananchi kuvamia hifadhi na kuua Wanyamapori huku wakipata utetezi toka kwa baadhi ya Wanasiasa.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej.Gen(Mstaafu) Hamisi Semfuko katika hafla ya kufunga mafunzo ya Kijeshi kwa watumishi 150 wa TAWA ikiwa ni utekelezaji wa mabadiliko ya utendaji kazi kutoka mfumo wa Kiraia kwenda wa mfumo wa Kijeshi.Mafunzo hayo yalifanyika eneo la Fort Ikoma katika wilaya ya Serengeti 22/12/2020.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi kutoka TAWA Bw.Mabula Misungwi alitoa shukrani nyingi Kwa Uongozi wa wilaya ya Serengeti na wadau wa Uhifadhi katika kuonyesha mshikamano wa dhati kuunga TAWA katika kupambana na ujangili.
Aidha.Bw.Mabula aliwataka wahitimu wakatumie ujuzi waliopata katika mafunzo hayo kuwa wazalendo ná kutojihusisha na vitendo vya rushwa.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Bw.Nurdin Babu amesema yupo tayari kushirikiana na TAWA katika kuhakikisha wananchi hawavamii maaeneo yaliotengwa kwaajili ya hifadhi.
"Sasa kazi ni moja tu, kupambana na changamoto dhidi ya Wananchi wanaovamia Mapori ya Akiba na Hifadhi za Taifa”
Mafunzo haya ya jeshi usu ni ya 11 kwa TAWA tangu mfumo wa kijeshi uanzishwe . Mfumo huu wa kijeshi umeleta mabadiliko makubwa kwa Watumishi tangu kuanzishwa kwake ambao umebeba picha ya Uzalendo.