KUSAYA: SIJARIDHISHWA NA KAZI YA MKANDARASI CHUO CHA KILIMO MUBONDO

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( aliyevaa fulana katikati) akikagua  vifaa vinavyotumika kukarabati hosteli ya wanafunzi wakati alipofanya ziara ya kushtukiza Chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MATI) Mubondo wilayani Kasulu leo. Kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho Bw. Hanif Nzully. 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( aliyevaa fulana katikati) akikagua  vifaa vinavyotumika kukarabati hosteli ya wanafunzi wakati alipofanya ziara ya kushtukiza Chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MATI) Mubondo wilayani Kasulu leo.  Katibu Mkuu huyo hajaridhishwa na kazi za mkandarasi Bogeti Engineering Ltd kutokana na kasi ndogo na ubora. 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( aliyevaa fulana katikati) akikagua  jengo la utawala linalokarabatiwa hosteli wakati alipofanya ziara ya kushtukiza Chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MATI) Mubondo wilayani Kasulu leo.  Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akikagua marumaru (tiles) wakati alipofanya ziara ya kushtukiza Chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MATI) Mubondo wilaya ya Kasulu leo ambapo hajaridhishwa na mwenendo wa mkandarasi Bogeta Engineering ya Dar es Salaam kutokuwa na ubora unaotakiwa hivyo ameagiza afanye maboresho.

************************************

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema atachukua hatua kali dhidi ya mkandarasi Bogeta Engineering Co. Ltd kutokana na kutekeleza mradi wa ujenzi wa ofisi na hosteli katika chuo cha mafunzo ya kilimo Mubondo wilaya ya Kasulu kwa kasi ndogo na ubora hafifu .

Katibu Mkuu huyo amesema hayo leo ( 16.12.2020) wakati alipofanya ziara ya kushtukiza chuoni hapo akiwa njiani kwenda Kigoma kwa ziara ya kikazi na kukuta mafundi wakiendelea na kazi lakini kwa spidi ndogo huku kukiwa na mapungufu ya ubora wa kazi yao.

“Sijaridhishwa na kasi ndogo ikiwemo ubora wa kazi hususan upande wa marumaru kuna mapungufu makubwa ya ubora, hivyo mwambeni mkandarasi afanye maboresho  ya kazi na ifikapo tarehe 15 Januari mwakani nahitaji anikabidhi kazi yangu ikiwa na ubora uliokusudiwa kwa mujibu wa mkataba” alisema Kusaya

Kusaya aliagiza mafundi hao wa kampuni ya Bogeta kuondoa kasoro ikiwemo marumaru kupishana, miundombinu ya umeme kutowekwa vizuri na pia kukamilisha kazi ya kupiga rangi majengo hayo ili ifikapo mwezi Januari mwakani yawe yamekamilika na kuanza kutumika.

Katibu Mkuu huyo alisema amefanya ukaguzi huo ili kujionea mwenendo wa mkandarasi huyo kufuatia ziara yake aliyoifanya chuoni hapo mwezi Mei mwaka huu ambapo aliagiza mradi huo uwe imekamilika hadi sasa.

“Nimekuja leo bila taarifa  lengo langu nimkute mkandarasi akiwa kazini na uhalisia wa kazi. Kwa kuwa hayupo mfikishieni salamu zangu kuwa sijaridhishwa na mwenendo wa kazi zake .Nataka spidi na ubora uongezeke ili mradi huu ukamilike mapema “alionya Kusaya.

Katibu Mkuu huyo wa Kilimo ameamwagiza msimamizi wa kazi ya ujenzi wa mradi huo kufikisha maelekezo kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Bogeta kuzingatia ubora na kuhakikisha mradi unakamilishwa vema.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MATI) Mubondo Hanif Nzully amesema mradi huo wa ukarabati wa ofisi ya utawala na bweni (hosteli) la wanafunzi ulianza mwezi mei mwaka 2019 na ulitarajiwa kukamilika ndani ya siku 60 .

Aidha, Nzully ameeleza kuwa mradi huo umegharimu fedha Shilingi milioni 367.3 ambapo utasaidia kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa watumishi na kuongeza nafasi ya wanafunzi kuishi chuoni hapo wakati wa mafunzo yao.

Wizara ya Kilimo inasimamia na kuendesha vyuo 14 vya mafunzo ya Kilimo (MATIs) pamoja na vituo vya mafunzo kwa wakulima vine ambapo seriklai ya Awamu ya Tano imedhamiria kufanya ukarabati wa miundombinu ya vyuo hivyo ili kuongeza uwezo na ubora wa utoaji mafunzo ya kisasa yatakayosaidia wanafunzi na wakulima nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post