Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aloycia Lyimo akimpima kiwango cha sukari mwilini mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo jana katika viwanja vya MwembeYanga wilayani Temeke kupitia jukwaa la One Stop Jawabu ambapo JKCI ilitoa bila malipo huduma za upimaji, matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo kwa watu 150.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sauli Philemon akimpima kiwango cha sukari mwilini mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo jana katika viwanja vya MwembeYanga wilayani Temeke kupitia jukwaa la One Stop Jawabu ambapo JKCI ilitoa bila malipo huduma za upimaji, matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo kwa watu 150.
Wananchi wakipata huduma bila malipo za upimaji, matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo kwenye banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika viwanja vya MwembeYanga wilayani Temeke kupitia jukwaa la One Stop Jawabu ambapo watu 150 walipata huduma, kati ya hao 37 walikutwa na shinikizo la damu kati yao 13 hawakuwa wanafahamu kama wanasumbuliwa na ugonjwa huo. Wawili walikutwa na tatizo la kutanuka kwa moyo mmoja akiwa na umri wa miaka 18, kisukari wanne na waliopewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo ni 13.Wagonjwa wote 37 walipewa dawa za kwenda kutumia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na wananchi waliofika kwenye banda la Taasisi hiyo jana katika viwanja vya MwembeYanga wilayani Temeke kupitia jukwaa la One Stop Jawabu ambapo JKCI ilitoa bila malipo huduma za upimaji, matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo kwa watu 150.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Godwin Gondwe aliyefika katika banda la Taasisi hiyo jana katika viwanja vya MwembeYanga kupitia jukwaa la One Stop Jawabu kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo zilizokuwa zinatolewa na Taasisi hiyo. JKCI ilitoa bila malipo huduma za upimaji, matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo kwa watu 150.
Mercy Kimaro kutoka kampuni ya dawa za binadamu ya Ajanta Pharm akitoa dawa kwa mwananchi aliyekutwa na tatizo la moyo mara baada ya kupata matibabu katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwenye viwanja vya MwembeYanga wilayani Temeke kupitia jukwaa la One Stop Jawabu ambapo watu 150 walipata huduma, kati ya hao 37 walikutwa na shinikizo la damu kati yao 13 hawakuwa wanafahamu kama wanasumbuliwa na ugonjwa huo. Wawili walikutwa na tatizo la kutanuka kwa moyo mmoja akiwa ni binti wa miaka 18, kisukari wanne na waliopewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo ni 13.Wagonjwa wote 37 walipewa dawa za kwenda kutumia
Wananchi wakisubiri kupata huduma bila malipo za upimaji, matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo kwenye banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika viwanja vya MwembeYanga wilayani Temeke kupitia jukwaa la One Stop Jawabu ambapo watu 150 walipata huduma, kati ya hao 37 walikutwa na shinikizo la damu kati yao 13 hawakuwa wanafahamu kama wanasumbuliwa na ugonjwa huo. Wawili walikutwa na tatizo la kutanuka kwa moyo mmoja akiwa ni binti wa miaka 18, kisukari wanne na waliopewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo ni 13.Wagonjwa wote 37 walipewa dawa za kwenda kutumia.Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimpima shinikizo la damu (BP) mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika viwanja vya MwembeYanga wilayani Temeke kupitia jukwaa la One Stop Jawabu ambapo JKCI ilitoa bila malipo huduma za upimaji, matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo kwa watu 150.
Picha na JKCI
*************************************
Septemba 24, 2020 – DAR ES SALAAM
Na Mwandishi maalum
Jumla ya watu 150 wamejitokeza na kufanyiwa uchunguzi na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), watu 37 kati ya hao wamekutwa na shinikizo la damu, 19 walikuwa hawajijui hali zao hapo kabla.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Samweli Rweyemamu alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari alipokuwa akieleeza tathmini kuhusu huduma ya uchunguzi na tiba waliyoitoa kwa wakazi wa Temeke, Septemba 18 na 23, mwaka huu, Viwanja vya Mwembe Yanga na Zakheem, kwenye Jukwaa la One Stop Jawabu.
“Mwamko na mwitiko wa wananchi umekuwa mkubwa, juzi kule Zakheem tuliona watu 103, pamoja na leo jumla tumeona watu 253, tumepima kisukari, uzito, shinikizo la damu na moyo kwa kutumia mashine ya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO), umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG) na kutoa dawa kwa watu tuliowakuta na matatizo ya moyo,” alibainisha.
Dk. Rweyemamu alisema miongoni mwa watu hao walikuwepo wanawake, wanaume, watu wazima, vijana na watoto.
“Wawili tumewakuta tayari moyo umetanuka, mmoja ni binti mwenye umri wa miaka 18, tunahisi alipata maambukizi ya bakteria ambayo baadae inaleta athari ya moyo kutanuka, tumempa rufaa kuja JKCI kwa uchunguzi zaidi,” alisema.
Alisema watu watatu kati ya hao waliowachunguza wamekutwa wana kisukari hali ambayo baadaye inaweza kuwaletea shida ya shinikizo la damu na kuathiri afya ya moyo kwa ujumla.
“Wengi tumewakuta na uzito uliokithiri uwiano wa uzito na urefu (BMI) zaidi ya 24, hii ni shida iliyopo kwenye jamii, tumewapa elimu wananchi jinsi gani waishi ili kujikinga dhidi ya magonjwa haya yasiyoambukiza,” alisisitiza.
Dk. Rweyemamu aliongeza “Tumewaelekeza jinsi ya kuishi ili kuepukana magonjwa haya, wazingatie mtindo bora wa maisha, ulaji bora, waepuke mafuta ambayo hayakidhi vigezo tunahimiza mafuta ya mbegu ikiwamo alzet.
“Tukiweza kuyatumia hayo na kuepuka zaidi yale yatokanayo na wanyama ambayo mwisho wa siku hutusababishia mishipa ya damu kwenye moyo kuziba, tutaepuka magonjwa haya,” alisema.
Alisema miongoni mwa watu waliowaona wapo pia ambao waliwakuta na shinikizo la juu la damu ambao wanatumia pombe kupita kiasi.
“Mmoja ametueleza anatumia chupa saba za bia kwa siku, tumemshauri ametuahidi kwamba anakwenda kupunguza kiasi hicho ili kulinda afya yake.
Tumewashauri pia kupunguza matumizi ya chumvi nyingi kwenye chakula, kuepuka ulaji wa lambalamba, soda na kunenepa mwili,” alisema.
Dk. Rweyemamu alisema kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya moyo duniani ambayo hufanyika Septemba 29, kila mwaka wanahimiza pia watanzania kuzingatia kuepuka matumizi ya chumvi kupita kiasi.
“Wasiache kabisa kutumia chumvi lakini wapunguze na waepuke kutumia ile ya kuongeza mezani, maadhimisho ya mwaka huu yamepewa kauli mbiu isemayo ‘Use Heart to Beat Heart’ yanahimiza sisi wataalamu kuwahudumia vema watu wanaofika kuchunguza afya na kutibiwa kwa sababu wanatuhitaji,” alibainisha.
Aliwakaribisha Watanzania katika Viwanja vya Tanganyika Parkers Septemba 29, mwaka huu ambapo maadhimisho ya kilele cha Siku ya Moyo Duniani yanatarajiwa kufanywa na Taasisi hiyo.
Wakizunguma kwa nyakati tofauti wananchi walipata nafasi ya kupima katika banda hilo waliishukuru Serikali ya wilaya ya Temeke kwa kuandaa jukwaa kama hilo ambalo limewapa nafasi ya kupata huduma mbalimbali za muhimu kwa wakati mmoja.
Mama Tausi Yusuph mkazi wa Temeke Mikoroshini alisema kuna baadhi ya watu katika jamii wanamatatizo mbalimbali ya kiafya lakini kutokana na uwezo mdogo wa kifedha walionao wanashidwa kwenda katika Hospitali kubwa kwa ajili ya kupata matibabu.
“Mimi nilipima miaka ya nyuma na kugundulika kuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu (BP) lakini nilishindwa kwenda Hospitali kubwa kutokana na kutokuwa na fedha za matibabu.Namshukuru Mungu leo nimefika katika banda la Taasisi ya Moyo nimepata huduma na kupewa dawa za kutumia”, alishukuru Mama Tausi .
“Nilikuwa na tatizo la msongo wa mawazo kwa muda mrefu na nilifikiria hali ile inaweza nisababishia magonjwa ya moyo. Leo nilipofika katika viwanja hivi kutafuta huduma ya cheti cha kuzaliwa nikasikia Taasisi ya Moyo wako hapa kwa ajili ya matibabu. Nashukuru baada ya kufanyiwa vipimo nimekutwa moyo wangu uko safi hauna tatizo lolote lile”, alisema Isaya Ngunwa mkazi wa Buza.